Producer na CEO wa Bhitz Music Group, Hermy B ameandika barua ya wazi akielezea yaliyowahi kutokea Bhitz, uamuzi na mpango wao mpya.
Nikiwa kama CEO wa B’hitz Music Group na Producer ambaye napigana kama
producers wengine kuusogeza muziki wa Tanzania katika level fulani,
sikupendezwa kabisa na jinsi ambavyo baadhi ya watu walivyoizungumzia
B’hitz na jinsi ambavyo baadhi yao wanaichukulia.
Kutokana na yote yaliyozungumzwa na baadhi ya wasanii ambao tulitofautiana nao
kikazi, wengi wametuchukulia kama sisi ni wagomvi na wanyonyaji.
Lakini ukweli ni kwamba hakuna msanii ambaye alishatengeneza faida ya kifedha
kwa B’hitz na wasanii hao walikuwa wakifanya kazi bila malipo yoyote na
hata walipokuwa wakifanya shows tulikuwa tukiwaachia pesa kwa kuwa
tulifahamu bado muda mzuri wa mavuno kulingana na ubinadamu, makubaliano
na malengo, hivyo hakuna ukweli kuhusu hilo.
Hata hivyo, tumeyachulia yote yaliyotokea kama sehemu ya changamoto katika
kazi hii ngumu ya muziki Tanzania ambayo kwa kiasi kikubwa watayarishaji
wa muziki hawafaidiki nayo kama ilivyo kwa wasanii ambao wamejaliwa
kuwa na ushawishi mkubwa zaidi kwa jamii na kuaminika mara moja kwa kile
wanachokisema kuhusu sisi pale tunapotofautiana.
Kwa bahati mbaya, mipango tunayopanga nao tunapokuwa studio ama makubalinao
mengi tunayoweka kwa ajili ya kazi zao hayajulikani kwa umma, na pindi
wanapoyakiuka na kusababisha sisi kurudi nyuma tunaonekana wakosaji na
wacheleweshaji wa maendeleo yao.
Naamini wasanii na sisi ndio tunaofahamu ukweli ni upi kati ya yote yaliyosemwa
kupitia media kwa kuwa tunafahamu wapi tumetoka pamoja, tulikubaliana
nini na wapi tulipotofautiana na yupi kati yetu aliacha reli ya
makubaliano.
It’s a new chapter, na tunawatakia kila la kheri wasanii wote waliopita B’hitz na milango
iko wazi kwa msanii yeyote wa Tanzania. Lengo letu ni kuendelea
kuisupport jamii yenye vipaji kwa maendeleo ya taifa hili linalosifika
kwa vipaji.
Nafasi ipo kwa wasanii wote walioondoka na kuacha kazi zao B’hitz, najua
wanajua ni muziki mzuri na tusingependa kuona ukipotea au tukiutoa kwa
kufuata ratiba tulizowekeana awali wakati ambapo wao hawapo.
Wasanii wanaweza kufuata nyimbo hizo na tutakuwa na makubaliano fair ili maisha
ya muziki tulioutengeneza kwa ubunifu wa hali ya juu yaendelee na
watanzania wafaidike kwa kuusikiliza.
Tunaamini uwezo wa Bhitz kuinua vipaji ambavyo havina majina makubwa na kuvifanya
‘brand’ ni baraka ambayo inabidi iendelee kwa vipaji vingine ambavyo
bado havijajulikana na vina uwezo mkubwa.
Hivyo, tunapenda kuuarifu umma wa watanzania kuwa Bhitz imefungua ukurasa mpya
na hatuendelei kuyashikilia tena matatizo yaliyokuwepo na wasanii hao.
Tunafurahi pia kuona muziki tuliotengeneza nao wakati tukiwa pamoja unawapa nafasi
kubwa na kuwasogeza katika ngazi nyingine, tunaamini wanatoa shukurani
zao kwa Mungu na zinatufikia kwa kiasi tunachostahili.
Tunaamini tutafika mbali na tumekomazwa zaidi na yaliyojiri kwa kuwa tumejifunza pia, yale ni mapito.
Music shall continue to live and flow in our bloods, we shall support
Tanzanian music and musicians with all our hearts, We shall not give up
because we are a part of this beautiful musical community in Tanzania.
Katika hatua nyingine, ningependa kuungana na producers wengine kuyatoa ya
moyoni pia kuhusu kilio cha watayarishaji wa muziki Tanzania ambacho
kimeendelea kuonekana kama kilio cha samaki. Huenda ni kutokana na
idadi yetu ndogo kulinganisha na wasanii hivyo kilio chetu hakina sauti
kubwa au ni mfumo mzima wa Industry ya Tanzania ulivyo mbaya na
umezoeleka!
Producers wengi Tanzania tumekuwa tukitumiwa na baadhi ya wasanii kama daraja la
mafanikio yao na kisha kutupaka matope au kuuambia umma kuwa sisi ndio
tumewakosea sana na tunawanyonya.
Laiti kama wasanii hao wangekuwa wanaeleza angalau mazuri wanayofanyiwa na
producers. Kwa bahati mbaya sifa wanazotumwagia tunapokuwa studio
tunafanya kazi huishia studio na umma husikia tu wimbo mzuri ukiwa
umetoka. Sifa zetu tunazopewa zimekuwa ‘perishable’ ingawa kazi
tunayofanya huishi miaka yote na hutumiwa na msanii husika.
*Kwa mazoea ya soko la Tanzania, producers wengi huwa na moyo wa mshumaa na
hata kuwatengenezea wasanii wetu midundo au nyimbo bure. Lakini wapo pia
ambao huwalipisha wasanii kiasi cha fedha ambacho kwa uhalisia wa kazi
na matunda ya kazi hii sio halali/sio fair bali ni bei zilizozoeleka tu.
Kwa uhalali wa ‘intellectual works’ wahusika wakuu huvuna matunda pamoja
kwa kugawana asilimia kila wakati ambapo kazi hiyo itakapokuwa ikiingiza
pesa. Lakini kwa Tanzania ni kama producer humuuzia haki miliki ya kazi
nzima msanii kwa shilingi kadhaa au hata bure na kisha msanii kuingiza
mamilioni kwa miaka mingi kwa kuuza au ku-perform kazi ile.
Hata kama ni kweli tasnia ya sanaa ya muziki kwa Tanzania bado inawanyonya
wadau kwa ujumla, kati ya hao wanaonyonywa tumkumbuke producer ambaye
yeye ananyonywa hadi damu ya mwisho na kisha kuchafuliwa pale
anaponyoosha mikono yote kutaka mambo yaende sawa.
Hebu fikiria, kama kweli mgao wa matunda ya kazi yangekuwa sawa kwa asilimia
kadhaa kwa kila kazi ambayo producer amefanya, producer kama P-Funk
Majani angekuwa na maendeleo kiasi gani kutoka kwenye muziki pekee?
Sisemi moja kwa moja kama aliofanya nao kazi walimnyonya, inawezekana
alinyonywa na mfumo ulivyo.
Lakini ni wasanii wangapi tumeshawasikia wakitaja mafanikio makubwa
waliyoyapata kwenye muziki kwa hits chache au hata hit moja tu. Je,
umeshajiuliza producer wake alipata nini?
Je, ni producers wangapi ambao wametengeneza hits kibao zilizowapeleka
wasanii mbali sana lakini wao wamebaki na hali ngumu kimaisha huku
wakiendelea kunyonga midundo na kuambulia sifa za studio?
Uzalendo na moyo wa pekee tuliopewa usiokata tamaa kwenye muziki huu ndicho kitu
pekee kinachotufanya tuendelee kuwekeza kwenye huu muziki na kuinua
vipaji vipya na kuendeleza vilivyopo kwa imani kuwa ipo siku tutavuna
matunda kwa kiasi tunachostahili.
Lakini kwa nini hiyo siku isiwe LEO? Itawezekana kama tutaungana na kuungwa mkono na wapenzi wa muziki mzuri.
Nisingependa kutaja majina ya producers wanaowalilia wasanii lakini karibia
producers wote wamekuwa wakifanya hivyo na vilio vyao hupuuzwa tofauti
na vilio vya wasanii.
Ndugu yangu Master Jay yeye amewahi hata kutoa kauli nzito kuwa wasanii ni wezi wanatuibia na
wanatunyonya sisi maproducer. Alikazia kuwa wizi huu wa wasanii ni wa
aina yake kwa kuwa huiba nguvu ya producers na kisha kujitangaza kuwa
wameingiza kiasi kikubwa cha fedha kwa kazi ile ile.
Lamar amewahi kusema wasanii wanapokuja studio huwa wapole na kukubaliana
mengi kuhusu wimbo lakini wimbo unapotoka na wao kufanikiwa huwasahau
kabisa producers walioumiza nao kichwa mwanzoni na hata ‘kuwavimbia’.
Lamar pia aliwahi kupata matatizo ya kimkataba na msanii wa Tanzania
ambaye aliamua kusaini tena na Candy n Candy ya Kenya ili hali akiwa na
mkataba mwingine.
Mikataba mingi tunayosaini nao mara nyingi huishia mikononi mwetu pale
wanapovunja japo sheria ya mikataba iko wazi lakini kiuhalisia wasanii
hao ni vigumu kulipa fidia itakayotajwa. Producer huamua kufunika kombe.
Producer Dupy yeye aliweka wazi kuwa sisi producers wa Tanzania ni masikini
kulinganisha na wasanii ambao tunafanya nao kazi na kueleza ukweli kuwa
hata wale wanaoonekana maisha yao ni mazuri ni wale ambao wanaingiza
kipato kupitia shughuli nyingine tofauti na muziki.
Mimi pia ni mmoja kati ya producers ambao wanapata fedha kupitia shughuli
nyingine na fedha hizo naziwekeza tena kwenye muziki kwa imani kuwa ipo
siku mambo yatakuwa mazuri lakini mara nyingi wasanii unaopanga nao
studio wanapopata mabawa (mafanikio) huruka na kueleza mabaya na sio
mazuri mliyofanya nao yaliyowapa hayo mabawa.
Sisemi kuwa sisi hatuwakosei wasanii, tunakoseana kwa kuwa sisi pia ni
binadamu japo sio kwa kiasi hicho wanachosema. Kukoseana katika kazi ni
jambo la kawaida. Kukwaruzana wakati wa ujenzi ni kawaida pia.
Lakini kwa kuwa msanii huyo tayari ni brand, hasara kubwa huwa kwa producer
ambaye inabidi aendelee kufanya kazi nyingine na watu wengine kwa
kuanzisha upya malengo yake huku akiwa amemfaidisha tayari msanii huyo
(Tayari ni brand).
Nyimbo tunazotengeneza nyingi studio tukisubiri msimu wa ‘mvua’ tuupush
zinapobaki huwa hasara kwa producer kwani wao wanaweza kwenda kwa
mwingine na wakazirudia. Je, producer anapata faida gani kwa kazi
aliyoifanya tayari?
*Imefika wakati ambapo producer inabidi aheshimiwe kwa sababu bila yeye
kusingekuwa na wasanii wengi wanaotamba hivi sasa. Hii itaongeza nguvu
pia ya kazi kwa producers wapya nchini.
Producer alipwe vizuri kwa sababu anapolipwa vizuri na yeye ubunifu na utendaji
wake wa kazi unakua kwa kiwango kikubwa. Pia atapata uwezo wa kununua
vitendea kazi bora zaidi vitakavyomsaidia kuingiza muziki wetu kwenye
ushindani wa soko la muziki Afrika na duniani kwa ujumla.
Naamini ipo siku hata haki za producer katika muziki alioutengeneza Tanzania
zitazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuvuna asilimia fulani ya muziki wake
pale unapotumika kwenye miito ya simu, na biashara nyingine.
B’hitz Music Group, inavishukuru vyombo vyote vya habari Tanzania kwa support
yao ikiwa ni pamoja na websites na blogs mbalimbali. Tuendelee
kushirikiana.
This is the time! Sisi tunaendelea na kazi na tunawakaribisha wasanii wote.
Regards.
Hermes B. Joachim
No comments:
Post a Comment