Baada ya majaji wa Mahakama ya Rufaa jijini Dar es Salaam kupitia hoja
za mawakili wa serikali na utetezi kwenye Rufaa ya hukumu ya kifungo cha
maisha jela katika kesi iliyokuwa ikimkabili mwanamuziki Nguza Viking
‘Babu Seya’ na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’, wameamua kuhairisha
rufaa hiyo mpaka tarehe husika ya kutoa hukumu ya kesi hiyo
itakapopangwa hapo baadaye
Katika rufani hiyo iliyosikilizwa na jopo la majaji watatu wa mahakama
ya rufani ambao ni Mbarouk mbarouk, Salum Massati na Nathalia
Kimaro,wakili wa upande wa mashtaka Mabele Marando amesema amekata rufaa
kutokana na kutosikilizwa kwa shahidi muhimu kwenye kesi hii ambae
alitajwa kuwa ndie aliwapeleka watoto hao kwa babu Seya.
Marando amesema pia ushahidi wa kuunga mkono ushahidi uliotolewa na
watoto haukuzingatia sheria baada ya mahakama kutembelea nyumbani kwa
babu Seya na kumuhoji mtoto bila ya kiapo hivyo ameomba Mahakama ipitie
upya hukumu hiyo ili kurekebisha kasoro zilizojitokeza.
Baada ya kuwasilishwa kwa maombi hayo,wakili wa serikali Jackson
Bulashi akiwa na wenzake wanne amepinga maombi yaliyotolewa na upande wa
mlalamikiwa na kubainisha kwamba hoja zilizowasilishwa Mahakamani
zilipaswa kuwasilishwa awali wakati kesi hiyo ilipokua inasikilizwa.
Wakili huyo wa serikali ameiomba Mahakama kutupilia mbali maombi hayo
kutokana na kutoainisha athari za moja kwa moja kwa washitakiwa na
kutaka adhabu ya kifungo cha maisha iliyotolewa dhidi ya babu Seya na
Papi Kocha iendelee kutekelezwa.
Baada ya pande zote mbili kutoa maelezo yao mbele ya jopo la majaji
watatu, Mwenyekiti wa jopo hilo Jaji Nathalia Kimaro ameahirisha kesi
hii ili kutoa nafasi kwa majaji kupitia maelezo yote yaliyotolewa na
kuyatolea maamuzi.
Babu Seya na Papi Kocha Mwaka 2004 walihukumiwa kifungo cha maisha
jela na hakimu mkazi Addy Lyamuya wa Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Dar
es salaam ambapo baada ya hukumu hiyo, February 2010 walikata rufaa
Mahakama kuu ya Tanzania ambayo iligonga mwamba mbele ya jaji Thomas
Mihayo wa Mahakama hiyo.

Mohamed Jaku
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment